Amesema kuanzia sasa, ofisi yake haiko tayari kupokea mwaliko wowote wa kushiriki au kuwa mgeni rasmi kwenye makongamano, pamoja na warsha kutokana na kutokuwa na faida kwa taifa.
Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wakati anazindua kiwanda kidogo cha kuzalisha chaki kinachoendeshwa na kikundi cha vijana cha Maswa Family Enterprises.
Amesema kutokana na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano, suala la mikutano, warsha na makongamano halina nafasi tena, na badala yake kinachohitajika ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kwa vitendo.
"Nitangaze kupitia uzinduzi wa kiwanda hiki, marufuku kuleta mwaliko wa warsha na makongamano ofisini kwangu, ofisi itakuwa tayari kupokea mwaliko wa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa vijana na jamii kwa ujumla," amesema Mhagama.
Amesema serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vijana wenye lengo la kujiletea maendeleo kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo kupitia umoja wao.
"Kuanzia leo kiongozi yeyote wa nchi hii asinialike kwenye kongamano, warsha au semina nitakuwa naalikwa kufanya kazi kama hii leo ya kufungua viwanda na miradi mingine," amesema.
Aliongeza kuwa, vijana wa kikundi cha kuzalisha chaki wameonesha njia kwa vijana wa Tanzania na wamefanya kumbukizi katika wiki ya vijana na kumbu,kumbukumbu ya Miaka 17 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumzia kiwanda hicho, Mhagama aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Simiyu kupitia Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka kuwa watendaji wa kwanza nchini kuanza kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli ya kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ikiwa pamoja na kuwasaidia vijana.
Alisema atawasiliana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kuona uwezekano wa serikali kupiga marukufu kuingiza chaki kutoka nje ya nchini.
0 comments:
Post a Comment