| mwenyekiti wa kamati ya LAAC vedasto ngombale mwiru |
SERIKALI imebainisha mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kuwa bado inamiliki kiasi kikubwa cha hisa katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Pamoja na hayo, wanahisa tisa wa Kampuni ya Simon Group yenye hisa milioni 3.6 kati ya hisa milioni 15 za shirika hilo, wametajwa rasmi mbele ya kamati hiyo akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Kaliua, Profesa Juma Kapuya.
Wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na viongozi wakuu wa Jiji la Dar es Salaam, waliwasilisha taarifa zao kuhusu sakata la umiliki wa UDA mjini Dodoma jana mbele ya kamati hiyo.
Wiki iliyopita, kamati hiyo ya LAAC, iliutaka uongozi wa Jiji ulioongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando, kuelezea namna kampuni hiyo ya Simon Group inayoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Robert Kisena, ilivyoingia na kuwa mmoja wa wanahisa wakubwa wa shirika hilo.
Hata hivyo, maelezo yaliyotolewa na uongozi huo wa halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ulishindwa kuwaridhisha wajumbe wa kamati hiyo na kuwataka, warejee tena siku ya jana wakiambatana na Waziri, AG na Msajili wa Hazina ili ukweli wa jambo hilo ubainishwe, ikiwemo wamiliki halali wa kampuni hiyo ya Simon Group.
Baada ya majadiliano hayo yaliyofanyika jana katika kikao cha ndani, Mwenyekiti wa kamati ya LAAC, Vedasto Ngombale Mwiru, wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema serikali imeitaarifu kamati hiyo kuwa tayari imerejesha hisa zote serikalini, zilizouzwa na kuibua mzozo kwa kampuni hiyo ya Simon Group.
“Kamati yangu imetaarifiwa na serikali kuwa hisa zote zilizokuwa hazijagawanywa (un allotted) asilimia 52 za UDA zilizouzwa kinyemela kwa kampuni ya Simon Group zimerejeshwa serikalini baada ya mgogoro wa kisheria wa muda mrefu baina ya serikali na kampuni hiyo,” alisema Mwiru.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka unaoishia Juni 2015, shirika la UDA lina jumla ya hisa milioni 15 ambazo kila moja imethaminishwa kwa jumla ya Sh 100.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa kati ya hisa hizo milioni 15, asilimia 47.5 sawa na jumla ya hisa milioni 7.1 ziligawanywa kwa makundi mbalimbali ambapo Jiji la Dar es Salaam lilipata aslimia 51 ya hisa hizo sawa na hisa milioni 3.6.
Makundi mengine yaliyogawanyiwa hisa ni serikali iliyokuwa na jumla ya hisa milioni 3.4 sawa na asilimia 49.
Ripoti hiyo, ilibainisha kuwa hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.5 ambazo hazikugawanywa za shirika hilo, ziliuzwa kinyemela na Bodi ya shirika hilo la UDA kwa Kampuni ya Simon Group ambazo tayari serikali imethibitisha kuzirejesha.
Kutokana na taarifa hiyo ya CAG na Waziri Simbachawene mbele ya kamati hiyo ya LAAC, kwa sasa serikali ina hisa nyingi zaidi katika kampuni hiyo kuliko wanahisa wengine. Hata hivyo, katika kutaka kuthibitisha kauli hiyo ya Serikali, kamati hiyo imempa muda wa wiki mbili Msajili wa Hazina, kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa hisa hizo kwa kamati hiyo.
Pamoja na hayo, mwenyekiti huyo, alisema pia katika kikao hicho, Msajili wa Hazina aliwataja wana hisa wa kampuni ya Simon Group pamoja na Kapuya anayemiliki hisa 10,000 wengine ni Robert Kisena hisa 94,000, Simon Kisena hisa 20,000, Gloria Kisena 20,000, William Kisena 10,000, George Kisena na Kulwa Kisena 10,000.
Kwa mujibu wa Mwiru, kamati hiyo pia iliamuagiza AG kutoa ushauri wa kisheria kuhusu namna ya kushughulikia Sh bilioni 4.6 zilizowekwa kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania, zinatokana na mauzo ya hisa za halmashauri ya jiji kwa kampuni hiyo ya Simon Group.
Hata hivyo, kwa sasa kuna mgogoro wa kisheria unaoendelea baina ya halmashauri hiyo ya jiji na Baraza la Madiwani kuhusu uhalali wa kuuzwa kwa hisa hizo, ambapo madiwani hao mpaka sasa wanaamini kuwa bado halmashauri hiyo ya jiji inamiliki hisa za shirika hilo la UDA.
Halmashauri hiyo ya jiji iliuza hisa zake kwa shirika hilo tangu mwaka 2013 baada ya Baraza la Madiwani kurudia na kampuni hiyo ilikuwa ikilipia hisa hizo taratibu kupitia akaunti hiyo ya BoT, ambapo hadi sasa fedha za hisa hizo zimefikia Sh bilioni 4.6.
Akizungumzia suala hilo la ushauri, Masaju aliahidi kuuandika kwa njia ya maandishi ushauri huo na kuukabidhi kwa madiwani hao utakaokuwa na maamuzi ya kisheria, lakini yenye tija kwa pande zote.
Akizungumzia sakata hilo ndani ya kikao hicho, Mafuru aliyataka mashirika yote ya umma, kujifunza kupitia sakata hilo na kuhakikisha kila wanapofanya uamuzi wa masuala makubwa kuzingatia suala la ushirikiano.
0 comments:
Post a Comment