| Gavana wa BoT prof. Beno Ndullu |
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imechukua usimamizi wa benki ya Twiga Bancorp Ltd kutokana na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki, ambapo hivi sasa benki hiyo inajiendesha kwa hasara ya Sh bilioni 21.
Kutokana na hatua hiyo, BoT imevunja Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya benki hiyo na kwamba ndani ya wiki moja watasitisha huduma kwa lengo la kujipanga jinsi ya kuendesha benki hiyo.
Akitangaza uamuzi huo jana jioni kwa waandishi wa habari Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndullu alisema sababu ya uamuzi huo inatokana na benki hiyo kuendeshwa kinyume cha sheria inayopaswa kufuatwa na benki zote, kuna upungufu mkubwa wa mtaji ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha.
“Tunajua benki hii inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100, tulizungumza nao kwa muda sasa inaonekana mtaji wa kuiongezea benki hii hautatolewa tena, kwa hiyo mamlaka inampa gavana kutoa kipindi cha benki kama hiyo kutafuta mtaji na sasa ni wazi kuwa haiwezi kupata mtaji huu tena, tumeamua kuiweka chini ya usimamizi wetu kujaribu kutafuta suluhu ya kuendesha benki hiyo,” alisema Gavana Ndullu.
Alisema uamuzi wa BoT umekuja ili kulinda wateja wa benki hiyo waliowekeza fedha zao pamoja na kulinda usalama wa benki nyingine kwa sababu inapotokea hali kama hiyo kwenye benki moja, kama hatua hazitachukuliwa inaweza kusababisha benki nyingine kuanguka.
Gavana Ndullu alisema hatua hizo ziko ndani ya Sheria namba 56 (1), (g) (i) na 56 (2) (a)-(d) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kwamba, pamoja na kuwa benki hiyo ina mali, lakini ina madeni mengi kuliko mali.
Hata hivyo alisema benki hiyo imekuwa ikipewa mtaji na serikali lakini pamoja na kupewa mtaji huo, bado inajiendesha kwa hasara na kusema kama kuna mwekezaji anayetaka kuweka mtaji kwenye benki hiyo anaweza ili kuiendesha.
“Kama kuna wanaotaka kuwekeza mtaji kwenye benki hii wanaweza na kubadili hali ya benki hiyo kwa sababu BoT haina mpango wa kuiendesha kwa muda mrefu, hiki tunachofanya ni kujaribu kupata suluhu kutoka kwa wawekezaji wengine, ila kama itashindikana kupata mwekezaji zipo njia nyingine za kufanya ili kile kilichopo wale wanaostahili wakipate,” alisema Gavana Ndullu.
Hata hivyo, aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa hali ya uchumi katika sekta za mabenki nchini ni nzuri kwa vigezo vya mtaji kwa sababu kiwango kinachotakiwa cha mtaji kulingana na aina ya biashara wanazofanya ni asilimia 10, lakini wao wamevuka na wana asilimia 18 na kwamba tatizo la Benki ya Twiga ni la muda mrefu na ndio maana wameamua kuchukua hatua sasa.
Alisema mtaji wa sasa wa benki hiyo ni hasi, na kwamba benki pamoja na kutoa huduma ndogo ndogo, lakini haijaongeza mtaji wa kujiendesha kwa muda mrefu.
Awali benki hiyo ilianza na mtaji wa Sh bilioni 7.5 na kwamba mwaka 2014 serikali iliongeza mtaji ila madeni yalikuwa makubwa na mengine hayakusanyiki hivyo kufanya hali ya benki kuwa mbaya.
Kuhusu wafanyakazi, Gavana Ndullu alisema wataendelea kuwepo kwa sababu kinachobadilika ni Msimamizi wa Benki ambaye atashughulika na watumishi na kuwatoa hofu kuwa wao si sehemu ya menejimenti hivyo wataendelea kuwepo.
Hata hivyo, Gavana Ndullu aliwaonya wale wote wanaodaiwa na benki hiyo kuhakikisha wanarejesha fedha walizokopa, kwa sababu sheria ina mkono mrefu na watasakwa popote ili kulipa fedha walizokopo na ikibidi mali zao kushikiliwa ambazo waliweka dhamana.
0 comments:
Post a Comment