Mtalam wa masuala ya moyo Professor Mohamed Janabi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete amefafanua namna ambavyo matukio ya matatizo ya moyo yanavyoweza kujitokeza kwa wanamichezo wanapokuwa uwanjani na kutoa ushauri kwa TFF namna ya kukabiliana na matatizo kama hayo.
Hii imetokana na tukio la mchezaji wa U20 wa timu ya Mbao FC Ismail Mrisho Khalfan aliyepoteza maisha Disemba 4 katika mchezo kati ya Mbao FC dhidi ya Mwadui FC kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Marehemu Ismail Khalfan alianguka ghafla uwanjani na kufariki muda mfupi wakati akipatiwa huduma ya kwanza ndani ya uwanja.
Kwa mujibu wa taarifa za madaktari wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera waliomfanyia uchunguzi Ismail Khalfan, imeonesha moyo wa marehemu ulisimama ghafla (Sadden Cardiac Arrest).
“Kifo kama kilichotokea kwa kijana Ismail Khalfan ni tukio kama la tatu au la nne hapa Tanzania lakini muhimu ni kutazama rekodi ya FIFA. Tangu kwaka 2006 FIFA ilianzisha kitu kinaitwa ‘Pre-Competition Medical Screening’ yaani mashindano yoyote yanayohusiana na FIFA lazima wachezaji wapimwe kabla,” amesema Prof. Janabi.
“Ukiangalia tafiti walizofanya FIFA katika nchi 170 ambazo ni wanachama wa FIFA, katika nchi hizo walikuta wachezaji 107 wanaanguka na kufariki (maana yake kila mwezi kuna mchezaji anaanguka na kufariki) ndiyo maana FIFA wakaja na hii sheria.”
“Tukio hili la kijana kufia uwanjani mimi nililiona kwenye TV kupitia taarifa ya habari, ukisikiliza utaratibu wa FIFA, nje ya uwanja kunatakiwa kuwa na mashine moja ya umeme ya kushtulia moyo. Kwasababu kinachotokea pale ni aidha moyo unasimama au mapigo yanakwenda vibaya, sasa ni lazima kile kifaa kiwepo kwa kila kiwanja wakati wa hizi mechi kwasababu unaweza kukiweka kwenye kifua kikapiga umeme kwenye kifua moyo ukanyanyuka.”
“Muda umefika sasa tujikumbushe sheria za FIFA, kwa mujibu wa sheria za FIFA mchezaji akianguka, madaktari hawatakiwi kusubiri mwamuzi awaambie waingie uwanjani kama ilivyotokea kwenye tukio la Ismail Khalfan. Wanatakiwa kumjulisha mwamuzi wa nje na kwenda moja kwa moja uwanjani kwasababu matatizo ya moyo kuna sekunde chache unatakiwa kufanya kitu flani la sivyo utampoteza mgonjwa.”
“Nilichokiona pale walianza kumvua soksi wakawa wanamnyoosha miguu kakuna mtu aliyemgusa kifuani ghafla tukaona kimya wachezaji wanzake wakaanza kulia.”
Kitu gani kilitakiwa kufanyika kwenye tukio la Ismail kuanguka uwanjani?
“Kitu cha kwanza ni kukimbia pale uwanjani na kuifungua mashine (ambayo ni ndogo ina kama nusu kilo), unaibandika kifuani itaonesha kama moyo umesimama au mapigo yanakwenda vibaya. Ile mashine ingempiga shock na kustua moyo baada ya hapo anakimbizwa kwenye ambulance yenye vifaa ambavyo vinaweza ku-monitor baadhi ya mambo kama oxygen na kumkimbiza hospitali kuendelea na matibabu mengine.”
Ushauri wa Prof. Jenabi kwa TFF
“Kuna taasisi kubwa kama ya Jakaya Kikwete tufanye utaratibu tuwasiadie TFF kwasababu hivi vitu kama tukishirikiana na wenzetu wa emergency medicine, tunaweza kuwafundisha na hivi vifaa vinagawiwa bure na FIFA au vinaweza kununuliwa hapahapa nchini kwasababu vipo hivyo vifaa lakini bahati mbaya kwa utaratibu huu tutaendelea kupoteza vijana wetu.”
“Kwa kuanzia, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili tungeanza na hawa wachezaji wa Premier League wa timu zote 16 wakafanyiwa vipimo vya kina haitachukua zaidi ya saa moja kwa mchezaji mmoja.”
0 comments:
Post a Comment