AKIFUNGA maadhimisho ya miaka 35 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mapema wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inaendelea kufanya utafiti wa taarifa za waombaji wa mikopo ya elimu ya juu, inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Aliahidi kuwa, kufikia siku ya Alhamisi asilimia 90 ya waombaji wa mikopo hiyo, ambao walitimiza masharti, wangekuwa wameshalipwa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa bodi hiyo, kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba wale ambao uhakiki wao umekamilika, wapatiwe mikopo hiyo kwa wakati na kwamba kamwe serikali haitawavumilia watumishi watakaochelewesha kwa makusudi mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Waziri Mkuu alisema kama kuna tatizo juu ya utoaji wa mikopo, taarifa itolewe haraka kwa serikali ili ifanyiwe kazi, kuzuia mgogoro kati ya wanafunzi na serikali yao. Hivyo, tunapongeza hatua ya Bodi hiyo, kuanza kutekeleza agizo hilo la Waziri Mkuu, ambapo ilipofika Alhamisi bodi ilitangaza kuwa imeingiza fedha za wanafunzi wote wa vyuo vikuu, ambao wamekidhi vigezo vya kupatiwa mikopo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru, wanafunzi 20,183, ambao wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), ndio ambao wamepata mikopo hiyo, baada ya kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa. Badru alisema Bodi imetimiza wajibu wake, hivyo waombaji waende benki kuchukua fedha zao, baada ya benki husika kukamilisha taratibu zake.
Hata hivyo, Badru anaeleza kuwa kuna nafasi za wanafunzi 5,534 ambazo zimeachwa wazi kwa ajili ya waombaji waliochelewa kupata udahili, au wale wale ambao wamekosa mikopo, halafu wakakata rufaa na kushinda. Tunaomba waliobahatika kupata mikopo hiyo, kuitumia vizuri vyuoni kusoma kwa bidii hadi wahitimu masomo yao kisha kutumikia Taifa.
Lakini, tunawakumbusha wanufaika wa mikopo waliohitimu na kuanza kufanya kazi, kurejesha mikopo hiyo. Tunatoa tahadhari hiyo kwa sababu kuna wanufaika wengi wenye vipato vizuri hivi sasa, ambao hawataki kurejesha fedha hizo.
Tunaunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ya kuomba wanufaika wote wa mikopo, warejeshe haraka fedha hizo ili ziwasaidie wananchi wengine kupata elimu.
Aidha, tunaomba wanafunzi waliokopeshwa mwaka huu, waepuke migomo na vurugu watakapokuwa chuoni kwa sababu ikitokea wakafukuzwa, lazima fedha hizo za serikali wazirejeshe.
Wanafunzi wanapofanya migomo, watambue kuwa wamechukua mikopo ya serikali, hivyo ikitokea wakafukuzwa, fedha hizo za serikali lazima zirejeshwe. Wanafunzi waache kufikiri kuwa wakifukuzwa, hizo fedha zitakuwa ndiyo basi.
0 comments:
Post a Comment