Na Baraka Mbolembole
MECHI 7 za ligi kuu ya kandanda Tanzania Bara ( VPL) zinataraji kuchezwa Jumatano hii. Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga SC wataikaribisha Mtibwa Sugar FC ya Turiani, Morogoro katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Makamu bingwa, Azam FC watakuwa katika ‘majaribu’ ndani ya uwanja wa Kambarage, Shinyanga dhidi ya wenyeji Stand United.
Mbeya City FC itawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mipambano hiyo mitatu itafuatiliwa sana kutokana na kwamba timu hizo 6 zipo katika nafasi 7 za juu.
YANGA v MTIBWA
Yanga iliifunga Mtibwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 6 katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro msimu uliopita, na wakaichapa tena katika game ya marejeano katika uwanja wa Taifa mapema mwaka huu na kuvuna pointi zote 6 kwa mara ya kwanza kutoka kwa ‘Wakata Miwa’ hao wa Turiani tangu mwaka 2008.
Safari hii wanakutana katika game ya raundi ya 8 na Mtibwa wapo juu ya Yanga kwa alama tatu zaidi. Yanga imecheza game 6 hadi sasa na imekusanya alama 11. Wapo katika nafasi ya 6 ya msimamo.
Mtibwa baada ya kupoteza michezo miwili ya nyuma, chini mkufunzi, Salum Mayanga imeanza kukaa sawa huku washambuliaji wake, Rashid Mandawa na Haroun Chanongo wakianza msimu vizuri.
Wawili hao wamekwisha funga jumla ya magoli matano kati ya 8 yaliyofungwa na timu hiyo. Mandawa ambaye amesajiliwa akitokea Mwadui FC tayari amefunga magoli matatu wakati Chanongo aliyejiunga na timu hiyo akitokea Stand United yeye amefanikiwa kuifungia timu yake magoli mawili.
Wanakutana na safu bora zaidi ya ulinzi katika VPL. Yanga imeruhusu magoli mawili tu hadi sasa na ndiyo timu iliyoruhusu magoli machache zaidi katika ligi miongoni mwa timu zote 16 msimu huu.
Kikosi cha Mholland, Hans Van der Pluijm kinaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kuangusha pointi nne katika game mbili za mwisho. Walipoteza ugenini, Stand United 1-0 Yanga kisha wakashindwa kulinda uongozi wa muda mrefu katika game vs Simba ambayo ilimalizika kwa sare ya timu hizo kufungana 1-1.
Wanakutana na Mtibwa huku safu yao ya mashambulizi ikiwa imefanikiwa kufunga magoli 9. Amis Tambwe, mfungaji bora wa VPL msimu uliopita amefunga mara nne na kiungo wa pembeni, Deus Kaseke amefanikiwa kufunga magoli mawili hadi sasa.
Itakuwa mechi ngumu kwa kila upande na mbinu za makocha zinataraji kuamua matokeo ya game hii.
0 comments:
Post a Comment