| Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakina mpango wa kukaa meza moja ya mazungumzo na Chama cha Wananchi(CUF) katika hoja ya uchaguzi mkuu pamoja na kuwepo kwa serikali ya mpito kwani uchaguzi wa marudio uliomuwezesha Dk Ali Mohamed Shein kuwepo madarakani ulikuwa huru na haki.
Hayo yalisemwa na Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa kwamba CUF wapo tayari kuzungumza na CCM katika suala la ajenda ya uchaguzi mkuu uliopita.
Vuai alisema uchaguzi mkuu wa marudio ulikuwa huru na haki baada ya kuthibitishwa na ZEC na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amechaguliwa kihalali kuiongoza Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2020.
“Wanachama wetu wa CCM msiwe na hofu hakuna mazungumzo yanayofanywa na wapinzani CUF kuhusu uchaguzi mkuu wa Machi 20 mwaka huu, uchaguzi ulikuwa huru na hakuna serikali ya mpito,” alisema.
Alifahamisha kwamba CCM ipo tayari kuzungumza na viongozi wa chama hicho katika ajenda nyingine ikiwemo za kuleta amani na utulivu pamoja na kujenga nchi na mshikamano wa wananchi wa Unguja na Pemba.
Aliwataka wanachama na wafuasi wa CCM kuondoa hofu kuhusu kauli hiyo ya wapinzani ambayo lengo lake kubwa ni kujaribu kuwababaisha wananchi pamoja na kujenga matumaini kwa wafuasi wao ambao wamekuwa wakiwadanganya kwa muda mrefu.
Akifafanua zaidi, Vuai alisema CCM pamoja na viongozi wake wanakabiliwa na mikakati na malengo manne makubwa ikiwemo kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM iliyonadiwa na Rais John Magufuli pamoja na Rais Shein, wabunge na wawakilishi.
Aidha alisema kwa sasa CCM ipo katika matayarisho ya uchaguzi wa chama wa mwaka 2017 ikiwemo kuweka kanuni vizuri zitakazosimamia utekelezaji wa chama.
Mikakati na malengo mengine ni kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kuhakikisha chama kinaendelea kushika hatamu ya kuongoza dola kwa mujibu wa katiba ya chama.
“Hiyo ndiyo mikakati na malengo yetu kuhakikisha tunasimamia ilani ya chama iliyotuweka madarakani lakini pia tunajipanga kwa uchaguzi wa ndani ya chama mwaka 2017 na kuhakikisha tunashinda katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli katika ziara yake ya siku mbili iliyomwezesha kufika Unguja na Pemba, aliwataka wananchi wasiwe na hofu wala wasiwasi kwamba Dk Shein ndiye rais halali wa Zanzibar na uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka huu ulikuwa huru na haki.
0 comments:
Post a Comment