Jaji Sivangilwa Mwangesi alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja za pande zote mbili katika shauri hilo na kukubali zilizowasilishwa na mawakili wa NHC.
Katika maombi hayo, Mbowe kupitia Kampuni yake ya Mbowe Hotels Limited, alifungua shauri namba 722/2016 dhidi ya NHC, akiiomba Mahakama itoe amri ya kurejeshwa katika jengo hilo kwa madai aliondolewa kinyume cha sheria.
Alidai NHC haikumpa ilani (notisi) kumtaarifu kama anatakiwa kuondoka katika jengo hilo, walimuondoa bila amri ya mahakama, pia Kampuni ya Udalali ya Foster (Foster Auctioneers and General Trad ers) iliyomuondoa katika jengo hilo haikuwa halali.
Aidha, aliiomba mahakama iamuru arudishiwe mali zake zilizochukuliwa na NHC kupitia Kampuni ya Foster kwa madai zilichukuliwa kiholela, pia itoe amri ya kuzuia asisumbuliwe baada ya kurudishwa.
Akitoa uamuzi jana, Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa hakukuwa na ubia kati ya kampuni hiyo na NHC, bali uhusiano uliokuwepo ni wa mpangaji na mpangishaji.
Aidha, mahakama imejiridhisha kuwa NHC ilifuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kupitia ilani ya siku 30 iliyotolewa mara mbili na baadaye siku 14.
Kuhusu uhalali wa kampuni ya udalali ya Foster, Jaji Mwangesi alisema haina mashiko kwa sababu NHC iliitumia kampuni hiyo kihalali kupitia baraza la ardhi, na kama kungekuwa na tatizo, walitakiwa wawasiliane na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.
Alifafanua kuwa, “kuna aina mbili za kampuni za aina hiyo, zinazosajiliwa na Mahakama (Court broker) pamoja na zinazosajiliwa na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi (Tribunal broker) na Kampuni ya Foster imesajiliwa na baraza”.
Hata hivyo, Mbowe kupitia mawakili wake Peter Kibatala, John Mallya na Omary Msemo wameomba wapewe nakala ya uamuzi ili wakate rufaa kupinga uamuzi huo.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Mallya, alisema hawajaridhishwa na uamuzi huo hivyo wanatarajia kukata rufaa, pia wamewasilisha maombi ya kuzuia NHC isifanye chochote katika jengo hilo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi wa rufaa yao.
Kwa upande wake, Wakili wa NHC, Aliko Mwamanenge aliishukuru mahakama kwa kutenda haki na kukubali kuwa mchakato wa kumuondoa Mbowe ulifanyika kihalali, hivyo mali zake haziwezi kurudishwa hadi atakapolipa deni analodaiwa.
Katika madai ya msingi ya Mbowe, alidai yeye siyo mpangaji katika jengo hilo, bali ni mbia ambaye anamiliki asilimia 75 katika uendeshaji wake na NHC wakimiliki asilimia 25.
Aidha, alidai hata kama angekuwa anadaiwa kodi, NHC ilimuondoa bila kufuata taratibu za kisheria kwa sababu hakukuwa na amri ya mahakama inayowapa wadaiwa nguvu ya kisheria ya kumwondoa.
Alidai kwa mujibu wa mkataba wa ubia wa pande hizo mbili, anapaswa kuwalipa NHC mapato ya jengo kila mwezi na kudai kuwa hadaiwi fedha yoyote kwani amekuwa akitekeleza matakwa hayo ya kimkataba kama yalivyosainiwa mwaka 1997, huku akiambatanisha ushahidi wa risiti ya fedha ambazo amekuwa akilipa.
0 comments:
Post a Comment